MORRISON 'ATUA' SPUTANZA

Winga wa Yanga Benard Morrison

Na Arone Mpanduka, DAR ES SALAAM

Chama cha wachezaji wa soka nchini (SPUTANZA) kimezipokea taarifa za utovu wa nidhamu za winga wa Yanga Benard Morrison kwa masikitiko makubwa na kusema kwamba mchezaji huyo amejishushia hadhi yake.

Julai 12 mwaka huu, winga huyo mwenye uraia wa Ghana aliondoka uwanjani moja kwa moja wakati mchezo wa watani wa jadi ukiendelea wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA.

Morrison aliondoka uwanjani kinyume na utaratibu baada ya kufanyiwa mabadiliko na kocha Luc Eymael, kwani alipaswa kwenda kuketi katika benchi la wachezaji wa akiba lakini yeye alilipita benchi hilo na kisha kwenda kubadilisha nguo kwenye vyumba vya kupumzikia na kuondoka zake.

Akizungumza na Mchakamchaka hivi karibuni Mwenyekiti wa SPUTANZA Musa Kisoki alisema kwa mujibu wa kanuni mchezaji huyo hakupaswa kuondoka wakati mechi ikiwa inaendelea kwani alikuwa akihesabika kama sehemu ya mchezo.

“Mchezaji unapokuwa katika benchi la wachezaji wa akiba unahesabika upo mchezoni kabla na baada ya kucheza mechi, ndiyo maana utaona hata wakati anatoka, mwamuzi wa akiba alikuwa anasukumana nae akimkatalia kuondoka.Tumesikitishwa sana na kitendo alichofanya,”alisema Kisoki.

Alisema mbali na tukio hilo, SPUTANZA imekuwa ikisikia vituko vingi vya mchezaji huyo katika klabu yake ambavyo vinaonyesha utovu wa nidhamu kwa kiasi kikubwa, lakini wanaiachia Klabu kwakua ndiyo yenye maamuzi kwa mchezaji husika.

“Hilo suala hatutaki kuiingilia klabu, mchezaji ni mali ya klabu, hivyo wao wana mamlaka ya kuamua nini cha kufanya ingawa sheria na kanuni zipo wazi kwa mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu,”alisema Kisoki.

Mapema mwaka huu winga huyo aliwashtukiza mashabiki wa Yanga kwa kiwango chake maridhawa ukiwemo mchezo wake wa kwanza aliocheza Januari 22 mwaka huu dhidi ya Singida United klatika uwanja wa Liti mkoani Singida.

Katika mchezo huo Yanga ilishinda mabao 3-1 huku Morrison akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo hasa kwa pasi zake za mwisho.


Comments