SAMATTA, ALI KIBA WATUNISHIANA MISULI


Na Arone Mpanduka, DAR ES SALAAM

Msanii Ali Kiba pamoja na mshambuliaji wa Aston Villa ya Uingereza Mbwana Samatta wametunishiana misuli kuelekea mchezo maalum wa hisani utakaopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Mechi hiyo ambayo imeandaliwa na Taasisi ya SamaKiba, huchezwa kila mwaka kwa lengo kusaidia watu wenye uhitaji hasa wanafunzi ambapo Samatta huunda timu iitwayo Team Samatta huku Ali Kiba akiunda timu iitwayo Team Kiba.

Ali Kiba ambaye kikosi chake mwaka jana kilifungwa mabao 6-3, amesema safari hii hatokubali kunyanyaswa huku Samatta akiahidi kuendeleza rekodi ya kichapo kwa wapinzani wao.

Samatta tayari ameshatangaza timu ya watu watano ambao ni Mohamed Samatta, Idd Seleman ‘Nado’, Farid Mussa na Juma Kaseja na msemaji wake ni Haji Manara, ambaye ni Ofisa Habari wa Klabu ya Simba.

“Nina kikosi changu ambacho ninaamini kitafanya vizuri siku hiyo.Nitaendeleza ubabe wa kumchapa nyingi bwana Kiba.”alisema Samatta.

Kwa upande wa Kiba yeye kamtaja Juma Mgunda kuwa kocha wake na Mwalubadu kuwa msemaji huku wasanii wake wawili wa Kings Music, K2ga na mdogo wake Abdu Kiba wakitajwa kuwa sehemu ya kikosi hicho.

“Kocha wangu ni Juma Mgunda lakini kuna wachezaji wakali sana akiwemo Bakari Mwamnyeto, kwa hiyo nitamnyoosha Samatta siku hiyo.Uteja sasa basi,”alisema Kiba.


Comments